KIJANA JELA MIAKA 32 KWA UJAMBAZI NA KUPORA MALI.


 KIJANA JELA MIAKA 32 KWA UJAMBAZI NA KUPORA MALI.

 

Na Said Hamdani, LINDI.

 

Febuari 06:MAHAKAMA ya Hakimu mkazi Wilaya ya Lindi imemuhukumu mkazi Kata ya Ng’apa Manispaa ya Lindi Bashiru Anthony (21) kutumikia kifungo cha miaka (32) Gerezani, baada ya kupatikana na hatia ya makosa mawili likiwemo ujambazi wa kutumia nguvu na kuiba mali.

 

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu mkazi Mahakama hiyo,Dolfina Kimati baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashita.

 

Kabla Hakimu Kimati kutoa adhabu hiyo,mshitakiwa alipewa nafasi ya kujitetea na kuiomba Mahakama isimpe adhabu kali kwa madai ni mkosaji wa mara ya kwanza,ana mke,mtoto mdogo aliyezaliwa mwezi Disemba 2024 na mama yake ambaye ni mzee,hivyo kama atapewa adhabu kali watakosa huduma ake.

 

Baada ya utetezi huo,Hakimu Kimati alimuuliza mwanasheria wa Serikali Moffat Seth iwapo ana kumbukumbu za makosa ya zamani kwa mshitakiwa na kujibu hana,huku akaiomba Mahakama kumpa mshitakiwa adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine walio na tabia ya aina hiyo.

 

Seth alisema kitendo kilichofanywa na mshitakiwa kumchoma mlalamikaji Bisibisi Shingoni na kunyang’anya Pikipiki yake baada ya kumkodi ampeleke Shambani na kumfanyia unyama,jambo la hatari sana lisilostaili huruma,kwani kama asingepatiwa matibabu ya haraka angeweza kupoteza uhai wake.

 

Hakimu Kimati akitoa hukumu katika kesi hiyo namba 21/747/2024 kupitia vifungu vya Sheria 287 A na 225 kanuni ya adhabu Sura ya 16/2022,alisema amesikiliza maombi ya pande zote mbili,lakini kwa vile Sheria imemshika mkono,akamuhukumu kosa la kwanza kifungo cha miaka 30 la pili kujeruhi miaka miwili Gerezani .

 

Kutokana na adhabu zote kwenda kwa pamoja mshitakiwa atatumikia Gerezani Kifungo cha miaka (30) huku Mahakama ikiamuru Pikipiki kurejeshwa kwa mmiliki na Bisibisi iliyotumika kumjeuhi mlalamikaji imetaifishwa na kuwa chini ya mali ya Serikali.

 

Awali ilidaiwa na mwanasheria Seith aliiambia Mahakama kuwa mshitakiwa alifanya unyama huo Julai 17/2024,baada ya kumuomba Selemani Mussa Salum (20) mkazi wa Kata ya Ng’apa ambaye ni mwendesha Piikipiki kumchoma Bisibisi Shingoni kisha kumpora pikipiki yake aina ya HAOJUNE.

 

Mwanasheria huyo alisema baada kuipora na kuondokanayo,pikipiki hiyo yenye namba za usajili CM 835 EKJ aliitelekeza njiani baada kushindwa kuiendesha kutokana na kukwama kwenye matope na mshitakiwa kukimbilia Wilaya ya Nachingwea kujificha hadi alipokamatwa na kufikishwa Mahakamani.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments