TARURA yatoa wito wananchi watumie fursa zitokanazo na barabara.
Na Ahmad Mmow, Nachingwea.
Wananchi wameshauriwa wachangamkie na watumie fursa zinazotokana na kuwa na barabara nzuri na bora.
Wito huo umetolewa leo tarehe 24.08.2024 mjini Nachingwea na meneja wa wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA)wa wilaya ya Ruangwa,mhandisi Mashaka Nalupi baada ya kupokea maoni ya wananchi wa vijiji vya Mkumba, Mpiruka A na B kufuatia kukamilika upembuzi yakinifu wa ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami ya kutoka Nandagala hadi Nachingwea mjini yenye urefu wa kilometa 31.
Mhandisi Nalupi ambae wilaya yake inatekeleza mradi huo unaofadhiliwa na benki ya dunia, licha ya kuwaomba wananchi watoe ushirikiano ili kufanikisha mradi huo amesema ujenzi wa barabara hiyo na nyingine zilizopo kwenye mradi huo za Ruangwa-Nangurugai, Nangwego-Namkatila na Mandawa-Mkaranga utakuwa na fursa nyingi ambazo wananchi wanaweza kunufaika nazo.
Amesema wananchi waongeze kiwango cha uzalishaji. Kwani kuna uhakika wa kufikisha mazao yao sokoni kwa wakati. Lakini pia wanunuzi watakwenda kununua kutokana na kufikika kirahisi. Hali ambayo itasababisha bei ya mazao, hasa ya kilimo kuongezeka.
Alizitaja fursa nyingine kuwa ni zile zitakazo jitokeza wakati wa ujenzi wa barabara hizo na baada ya kukamilika ujenzi huo. Kwani mfadhili(benki ya dunia) anataka wafanyakazi hasa vibarua wa ujenzi huo wapatikane kutoka kwenye vijijiji ambavyo barabara hizo zinapita. Kwahiyo vikundi vya vijana na wanaweke vya uzalishaji mali vitanufaika kwa kufanya kazi hizo.
" Kipindi cha matazamio kabla ya kukabidhi barabara hizo mfadhili atatoa mafunzo na elimu ya kutunza na kulinda barabara hizo. Ambapo washiriki na walengwa wa mafunzo hayo watakuwa wananchi hasa vijana. Kwahiyo ni fursa nyingine ukiachilia mbali kusafiri kwa haraka na hata viwango vya nauli kupungua kutokana na ushindani wa biashara wa vyombo vya usafirishaji," alisema Nalupi.
Mtaalamu huyo wa ujenzi na matengenezo ya barabara alitoa wito kwa wananchi ambao wanaishi katika vijiji ambavyo mradi huo unatekelezwa watoe ushirikiano. Hasa kutoa maoni na ushauri ili kuepuka migogoro. Kwani nia kubwa ya mradi huo ni kupeleka maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi. Ndiyo sababu wananchi wanashirikishwa katika hatua zote za mradi huo.
Nalupi akieleza maendeleo na hatua zilizofikiwa na zinazo endelea za mradi huo wenye jumla ya kilometa 100 ambao pamoja nao kuna miradi mingine kama huo katika wilaya za Handeni, Kilolo, Mufundi na Iringa vijijini. Kwamba hatua iliyofikiwa sasa ni upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, kupokea maoni ya wananchi na baadae kufanya tathimini ya mali. Ambapo baada ya kukamilika hatua hizo benki ya dunia itatoa kibali cha kutangaza kandarasi. Kwani tayari gharama za ujenzi zitakuwa zimejulikana.
Amesema katika wilaya za Iringa kijijini, Mufindi na Kilolo ujenzi wa barabara hizo
umeanza.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mpiruka, Issa Makota(Ambuje) licha ya kuishukuru serikali alisema barabara hiyo itaongeza fursa za kujipatia kipato wananchi wa kata yake. Lakini pia zitapunguza kiwango cha nauli. Kwani kutoka Mpiruka kwenda mjini Nachingwea ni shilingi 7,000 kwa bodaboda .
" Barabara hii ikikamilika kwa kiwango cha lami gari zitakuwa nyingi. Hapa hadi mjini ni kilometa nane tu lakini tunalipa shilingi 7,000 kwa bodaboda. Kwa basi shilingi 2,000 wakati huo tutaweza kwenda kwa buku(shilingi elfu moja," alisema Ambuje.
Diwani huyo pia alitoa woto kwa wananchi kutokuwa kikwazo cha utekelezaji wa mradi huo. Bali watoe ushirikiano ili wanufaike na barabara hiyo.

0 Comments