Makota: Wanawake tuamke na tukatae kufanywa madaraja.
Na Ahmad Mmow, Nachingwea.
Wanawake wilayani Nachingwea mkoani Lindi wameaswa wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi mbali mbali za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu.
Wito huo ulitolewa jana na makamo mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea, Veronica Damaso Makota kwenye mkutano wa hadhara wa wanawake wa kata ya Mpiruka uliofanyika katika kijijji cha Mpiruka A.
Makota ambae ni diwani wa viti maalum(CCM) anaetokea kata ya Mpiruka yenye vijiji vya Mkumba, Libea, Mpiruka A na Mpiruka B, alisema wanawake wana nafasi kubwa ya kushinda chaguzi na kushika nafasi za uongozi iwapo watajitokeza kuomba na kuamua kuunganisha nguvu.
Aliweka wazi kwamba katika kata ya Mpiruka kwamfano, kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 idadi ya wanawake ni kubwa kuliko wanaume.
Kwa kuzingatia motekeo hayo ya sensa ya watu na makazi alisema wanawake wakiamua kupigiana kura nafasi zote zinawezakushikwa na wanawake.
Alisema kwa kukosa mshikamano na kushindwa kujitokeza kugombea nafasi, wanawake kwa miaka nenda miaka rudi wamekuwa kama madara ya kuwapitisha wanaume kuwa viongozi.
" Mwaka huu tuamke. Kwa wingi wetu sipobaguana tuna uwezo wa kuchukua nafasi zote. Halafu wanaume wabaki nyumbani kama sisi tulivyokuwa tunabaki nyumbani kutunza familia. Muda wa kufanywa madaraja umekwisha na tukatae," alisema na kuchekesha Makota.
Katika kusisitiza wito wake alisema atashangaa kusikia mwanamke atakae kugombea nafasi ya uongozi dhidi ya mwanaume ameshindwa. Kwani wanaume ni wachache kuliko wanawake.
Aidha kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) alitahadharisha kwamba utengano baina ya wanawake unaweza kuwafanya washindwe. Bali kama watapendana na kuwa kitu kimoja watashinda.
Aliweka wazi kwa kusema kwamba miongoni sababu za wanawake wachache wanaojitokeza kuomba uongozi kushindwa ni wanawake wenzao kuwadharau na kuwaona hawasitahili kuwa viongozi.
0 Comments