WAKULIMA WA UFUTA LINDI WAISHUKURU SERIKALI UNUNUZI WA KIDIGITALI.


Wakulima wa ufuta Lindi waishukuru serikali ununuzi wa kigitali.

Na Ahmad Mmow,  Lindi.

Wakulima wa ufuta wilayani Lindi ambao wanahudumiwa na chama kikuu cha ushirika cha Lindi Mwambao wameishukuru serikali kwa ununuzi wa ufuta kwa njia ya kidigitali.

Wakizungumza katika kijiji cha Zingatia, wilaya ya Lindi baada ya kukubali kuuza ufuta wao katika mnada wa saba kwa chama kikuu hicho kwa mwaka wa 2024, walisema mfumo huo umeziba mwanya wa dhuluma. Kwani ununuzi unafanyika kwa uwazi.

Mkulima Said Nanguka wa kijiji hicho cha Zingatia ambacho kipo kata ya Nnolela alisema serikali imefanya jambo jema kuagiza ununuzi wa  ufuta kutumia mfumo wa kiilektroniki ambao unafanywa na soko la bidhaa Tanzania(TMX) badala ya mfumo wa barua.

Hata hivyo mkulima huyo licha ya kuipongeza serikali alitoa wito iwawezeshe pembejeo na viatilifu wakulima wa zao hilo kama wakulima wa korosho.

Alisema ufuta una magonjwa mengi yanayosababisha uzalishaji kuwa mdogo. Hasa wadudu waharibifu. Kwahiyo ni vema serikali ikawawezesha viuatilifu ili waweze kuuwa wadudu.

Nae Zainab Omari mkazi pia wa kijiji hicho cha Zingatia alisema mnada kwa njia ya kiilektroniki umeondoa uwezekano wa rushwa na umeongeza uwazi.

Alisema kabla ya kuanza mfumo huo kutumika kulikuwa na dhana kwamba kulikuwa na dhuluma kupitia mfumo wa wazabuni kuomba kwa kutumia barua ambazo zilitumbukizwa kwenye masanduku ya zabuni na kufunguliwa siku ya mnada.

" Hatujui kama ni kweli au la. Lakini ununuzi na mnada wa aina hiyo umeondoa dhana hiyo. Maana wote tunaona wananunuzi wanavyoshindana bei," alisema Zainabu.

Nae Hamisi Libanda wa kijiji cha Nnolela  alisema sema mfumo huo wa ununuzi umeondoa lawama kwa serikali. Kwani kila kitu kipo wazi na wakulima wanashuhudia kinachofanywa na wanunuzi.

" Kwasasa serikali hailaumiki. Bei ikiwa  zikiwa ndogo ni wanunuzi wenyewe wameamua. Maana kila kitu kipo hadharani, sasa serikali italaumiwa nini?," alieleza na kuhoji Libanda.

Katika mnada huo bei ya juu ilikuwa shilingi  3,560 na bei ya chini shilingi 3,460. 

Post a Comment

0 Comments