JELA MIAKA 20 KUMILIKI NYARA ZA SERIKALI BILA KIBARI
Na Said Hamdani, LINDI.
Novemba 04/2024:MAHAKAMA ya Mkoa wa Lindi, imewahukumu watu wawili kati ya watatu Wilaya ya Liwale na kulipa faini ya Sh,1,741,200,000/-au kifungo cha miaka (20) Gerezani kila mmoja,baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki Nyara za Serikali Meno ya Tembo kinyume cha Sheria.
Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu mkazi mwandamizi Mahakama hiyo,Consolata Singano baada ya kuridhishwa pasipo na haka ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.
Washitakiwa hao Saidi Omari Nyayonga (39) na Abdallah Chande Mpingo (64) huku mshitakiwa wa tatu Rajabu Mohamedi Ngayonga (39) akiachiwa huru kwa kukosekana ushahidi wa kumtia hatiani.
Kabla kutolewa kwa hukumu hiyo,Hakimu Singano alimuuliza mshitakiwa iwapo anazo sababu za kuishawishi Mahakama isiwape adhabu kali kwa kosa linalowakabiri,kila mmoja aliomba isiwape adhabu kwa madai wanazo familia zinazowategemea.
“Mh Hakimu tunaomba Mahakama yako tukufu isitupe adhabu kali kwani tuna familia inatutegemea”Walieleza kila mmoja kwa wakati wake.
Baada ya utetezi huo,Hakimu Singano alimuuliza mwana sheria wa Serikali Denis Nguvu kama anazo kumbu kumbu ya makosa ya zamani kwa washitakiwa na kujibu hana,huku akiiomba mahakama kuwapa adhabu kali ili iwe fundisho kwao na wengine walio na tabia ya aina hiyo.
Nguvu alidai kitendo cha kuuwa Tembo watano bila kuwa na kibari kutoka kwa mamlaka husika ni kosa na uwaribifu wa rasimali ya Taifa la Tanzania ikizingatiwa ni moja ya uchumi mkubwa kwa Serikali yetu.
Hakimu Singano akitoa hukumu katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi Namba 02/2023 kupitia kifungu cha 86 (1) na 2 (b) ya Sheria ya uhujumu uchumi sura ya 283 rejeo la 2022 ikisomwa pamoja na haya ya 14 ya Jedwari la kwanza na kifungu cha 57 (1) na 60 (2) cha Sheria ya Uhujumu Uchumi sura 200 akawahukumu kila mmoja kulipa faini ya Sh,bilioni 1.741.200,000/-
Pia,Hakimu Singano akasema kama washitakiwa watashindwa kulipa faini hiyo wakatumikie kifungo cha miaka (20) Gerezani kila mmoja,huku akimuachia huru mshitakiwa wa watatu Rajabu Mohamedi Ngayonga (39) kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kumtia hatiani.
Awali ilidaiwa Mahakamani hapo na mwanasheria Nguvu kuwa washitakiwa walikamatwa Liwale B, Machi 07/2023 na askari Polisi wakiwa na idadi ya meno (10) ya Tembo yenye thamani ya Sh,Milioni 174,120,000/-tayari kwa ajili ya kusafirishwa Sokoni nje ya Wilaya na Mkoa.
Mwanasheria huyo aliieleza kwamba askari hao wakiwa kwenye Doria zao walipata taarifa kutoka kwa raia wema kuna watu wana meno ya Tembo yakisafirishwa,walipofuatilia wakafanikiwa kuyakuta Nyara hizo bila kuwa na kibari kutoka Mamlaka husika.
MWISHO.

0 Comments