Afisa mtendaji Songwe atupwa jela miaka ishirini.
Na Ahmad Mmow.
Mahakama ya wilaya ya Songwe, mkoani Songwe leo tarehe 18.11.2024 imekumta na hatia na kumuadhibu kwenda gerezani kutumikia kifungo cha miaka ishirini(20) afisa mtendaji wa kijiji cha Mbuyuni, halmashauri ya wilaya ya Songwe, Assan Jacob Kalinga.
Katika shauri hilo la Uhujumu uchumi namba 10/2023, Jamhuri dhidi ya Kalinga ilielezwa na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Simon Mapunda mbele ya hakimu mkazi mfawidhi, A.Lugome kwamba Kalinga alishitakiwa kwa kosa la ubadhirifu na ufujaji. Kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 28(1) cha sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, sura 329 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2022 ambacho kilisomwa pamoja na aya ya 21 ya jedwali la kwanza vifungu vya 57(1) na 60(2) vya sheria ya udhibiti wa makosa ya uhujumu uchumi na uhalifu wa kupangwa, sura ya 200 iliyofanyiwa mapitio mwaka 2022.
Mahakama hiyo ya wilaya ya Songwe baada ya kusikiliza maelezo(ushahidi) ya pande zote ambapo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 167 na vielelezo 13 ilijiridhisha pasipo shaka kwamba Assan alitenda kosa hilo. Hivyo kumtia hatiani na kumuadhibu kifungo cha miaka 20 gerezani.
Awali ilielezwa mahakamani hapo kwamba Kalinga afikishwa na kushitakiwa katika mahakama hiyo kutokana na kufanya ubadhirifu wa fedha kiasi cha shilingi 7,721,000, za wananchi wa kijiji cha Mbuyuni ambazo walichanga kulipia mita za umeme wa REA kati ya Mwezi Aprili hadi Oktoba 2020.

0 Comments