TUTATEKELEZA MAAGIZI YA WAZIRI MKUU KUHUSU WANAHABARI - NDEMANGA

 


Tutatekeleza maagizo ya waziri mkuu kuhusu wanahabari - Ndemanga

NA Ahmad A. Mmow

MKUU wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga,,amesema ofisi yake itakeleza kikamilifu maagizo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuhusu waandishi wa habari na vyombo vya habari alilolitoa wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Akizungumza na waaandishi wa habari na wadau wa habari kwa niaba ya mkuu huyo, Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Hudhaifa Rashid, alisema viongozi na watendaji walisikia vizuri hotuba ya Waziri Mkuu na maagizo aliyoyatoa katika maadhimisho hayo kuhusu waandishi wa habari.

“Maagizo ya Waziri Mkuu kwa waratibu wanaoandaa ziara za viongozi ikiwamo ofisi za Makatibu Tawala wa mikoa na wilaya kuhusu waandishi wanakuwepo kwenye ziara hizo wamepokea, wameyaelewa na watayafanyia kazi kwa vitendo”, alieleza.

Licha ya ahadi hiyo Rashid alitoa wito kwa waandishi wa habari kuandika habari sahihi na za ukweli ili serikali iweze kushughulikia habari hizo hususani zinazohusu kero na changamoto za wananchi.

Alibainisha kwamba hakuna tabia inayosababisha usumbufu kwa viongozi na watendaji wa serikali ni kuandika habari zisizo sahihi hivyo kuna haja ya wanahabari kuongeza ufuatiliaji wa ukweli kabla ya kutioa Habari hizo kupitia vyombo vya habari. 

"Tasnia hii muhimu sana. Andikeni habari za kweli, toeni elimu. Dunia inapita katika wakati mgumu kuhusu mazingira, mabadiliko ya tabia nchi na mambo mengine mengi," alisisitiza Rashid.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa klabu ya waandishi wa habari wa mkoa wa Lindi, Ahmad Mmow, alitoa wito kwa serikali itekeleze kwa vitendo sheria zinazohusu mazingira kwani licha kuwapo sheria nzuri lakini usimamizi na utekelezaji wa sheria hizo ni mdogo.

"Sisi kwa upande wetu tunakuahidi tutatimiza wajibu wetu kikamilifu. Bali serikali nayo isimamie utekelezaji wa sheria za mazingira zilizopo kwani kuna watu wanafanya shughuli za kibanaadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji na wengine wamepewa umiliki wa viwanja vya makazi na biashara katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kufanya shughuli za kibanadamu," alisema Mmow.

Nae Mwenyekiti wa klabu hiyo, Fatuma Maumba, alihimiza wadau wa Habari kuifanyia kazi kaulimbiu ya maadhimisho ya 31 ya tamko la Uhuru wa vyombo vya habari duniani kwani imekuja wakati muafaka. 

Alieleza kuwa dunia inapambana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi yanaonekana maeneo mbali mbali nchini huku chanzo chake ikiwa ni shughuli za kibinaadamu zikiwemo za ukataji wa miti na uharibifu ya mazingira.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ambayo yaliandaliwa na klabu hiyo kwa ufadhili wa Shirika la Misaada ya Maendeleo Kimataifa la Sweden (SIDA) kupitia Muungano wa Klabu za Wandishi wa Habari Tanzania (UTPC) chini ya kaulimbiu isesemayo; ‘Uandishi wa habari na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi’.

Post a Comment

0 Comments