TAKUKURU SONGWE YAMFIKISHA MAHAKANI AFISA UVUVI.

 


TAKUKURU Songwe yamfikisha mahakamani afisa uvuvi.


Na Ahmad Mmow,  Songwe.


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoani Songwe imemfikisha mahakamani na kumfungulia mashitaka ofisa uvuvi msaidizi wa kata ya Kamsamba, halmashauri ya wilaya ya Momba, Mussa Ladislaus Twaha.


Akisoma mashitaka yanayomkabili Twaha mbele ya hakimu wa mahakama ya wilaya ya Momba, Mheshimiwa Tagha Komba. Mwendesha mashitaka wa TAKUKURU mkoa wa Songwe, Hilda Mtaki alisema Twaha anakabiliwa na makosa mawili.


Wakili Mtaki aliyataja makosa hayo kuwa ni kutumia madaraka vibaya. Kitendo ambacho ni  kosa kwa mujibu wa kifungu cha k/f cha 31 cha PCCA, sura ya 329 ambayo ilifanyiwa marejeo mwaka 2022. Ambapo kosa la pili ni ufujaji na ubadhirifu wa fedha. Kitendo ambacho pia ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 28(1) cha PCCA, sura ya 329 ambayo pia ilifanyiwa marejeo mwaka 2022.


Mtaki alisema tarehe 16.04.2017 na 03.06.2019 Twaha akiwa na nia ovu alitumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kupeleka  fedha kiasi cha shilingi 12,744,010 kwa mhasibu wa halmashauri ya wilaya ya Momba. Kitendo ambacho ni kinyume cha agizo  namba 37(2) na 50(5) la randama  ya fedha za serikali za mitaa ya mwaka 2009.


" Mshitakiwa alifuja na kufanya ubadhirifu  kinyume cha kifungu 28(1) cha PCCA  sura ya 329 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022. Amefanya ubadhirifu wa shilingi 12,744,010 mali ya halmashauri ya wilaya ya Momba ambazo zilifika kwenye himaya yake akiwa mtumishi wa umma," Mtaki alibainisha.


Kesi hiyo imepangwa kuanza kusilizwa tarehe 14.05.2024. Ambapo Twaha ambae amekana mashitaka yote anaendelea kubaki mahabusu baada ya kushindwa kutekeleza masharti  ya dhamana.

Post a Comment

0 Comments