KIONGOZI WA MBI0 ZA MWENGE WA UHURU AWATAKA WAKULIMA WAACHE KILIMO CHA KUHAMAHAMA.


 

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru awataka wakulima waache kilimo cha kuhama hama.


Na Ahmad Mmow, Lindi. 


Wakulima nchini wametakiwa kuacha kilimo cha kuhama hama na wahifadhi  mazingira ili kuepuka uharibifu wa misitu, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi.


Agizo hilo limetolewa leo na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa 2024, Godfrey Mnzava katika kijiji cha Rutamba, wilaya na mkoa wa Lindi.


  Mnzava  amesema wakulima hawanabudi kuzingatia uhifadhi wa mazingira na kuachana na kilimo cha kuhamahama ambacho kimekuwa ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira.


Amewataka wakulima watazingatie kilimo cha kitaalamu  kwa kufuata maelekezo ya wagani wa kilimo  ambao wapo kila kata hapa nchini. Huku akikemea tabia ya uchomaji moto misitu. Kwani inaharibu jiolojia na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi.


Kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2024 alisema hayo baada ya kusomewa taarifa ya mradi wa kukabidhi  simu kwa jumuiya za uhifadhi wa  misitu kwa njia ya teknolojia  ili kuendeleza uhifadhi wa misitu  katika kijiji cha Rutamba.


 Alisema kuwa teknolojia hiyo isaidie kupambana na wanaovamia misitu kwa shughuli za kibinadamu. Huku akisisitiza kwamba  watakaobainika wachukuliwe hatua za kisheria.


Awali kwenye taarifa iliyosomwa na afisa mradi wa MKUHUMI, Nebby Nyale ilisema halmashauri ya manispaa ya Lindi kwa kushirikiana na shirika la kuhifadhi misitu ya asili iliwezesha vijiji 10 kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na kurasimisha misitu ya asili katika maeneo ya kiikolojia ya Noto, Rondo na  Chotoa. 


Taarifa hiyo ilisema kwamba mpango huo ni muhimu, kwani umeweza kudhibiti uharibifu kwa mafanikio makubwa kwa kutumia teknolojia ya simu janja iliyounganishwa na mifumo ya picha za angani.


Ilieza kuwa teknolojia hiyo inafanya  wataalamu wa ramani za uchambuzi wa picha za angani katika misitu ya vijiji kuweza kuainisha maeneo yenye uharibifu  mpya kila unapotokea.Huku ikibainisha kuwa katika manispaa ya Lindi teknojia hiyo imeanza kutekelezwa katika vijiji vya Kiwawa,Milola Magharibi,Kinyope,Ruhoma,Muungano,Mkombamoshi, Namkongo,Makumba  na Likwaya  ambapo zaidi ya doria 153 zimefanyika katika maeneo yote yaliyobainika kuwa na uharibifu mpya.


Mwenge huo wa Uhuru leo umeanza kukimbizwa katika halmashauri ya manispaa ya Lindi. Ambapo kesho utahitimisha  mbio zake katika mkoa wa Lindi baada ya kukimbizwa katika halmashari za wilaya tano na manispaa moja ambazo zipo katika mkoa huu wa Lindi.


Aidha kesho unatarajiwa kukabidhiwa na kupokewa katika mkoa jirani wa Mtwara.

Post a Comment

0 Comments