OFISA MTENDAJI WA KIJIJI SONGWE AFIKISHWA NA KUSHTAKIWA MAHAKAMANI NA TAKUKURU.

 


Ofisa Mtendaji wa kijiji Songwe afikishwa na kushitakiwa mahakamani na TAKUKURU.


Na Ahmad Mmow.


Ofisa mtendaji wa kijiji cha Nyambili halmashauri ya wilaya Mbozi mkoa wa Songwe, Neema Josiah Shari tarehe 07.06.2024 amefikishwa mahakamani na kufunguliwa mashitaka mawili.


Akisoma mashitaka hayo yaliyopo kwenye shauri la jinai namba 15544/2024 mbele ya hakimu mkzi wa mahakama ya wilaya ya Mbozi, Mheshimiwa Vitalis Changwe, mwendesha mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) mkoa wa Songwea , Hilda Mtaki alisema Shari ameshitakiwa kwa kutuhuma za kutenda makosa mawili ambayo anatakiwa kujibu katika mahakama hiyo.


Mtaki aliyataja makosa hayo kuwa ni kutumia madaraka vibaya na ufujaji na ubadhirifu. Huku akibainisha kwamba Shari alitenda makosa hayo tarehe 09.08.2017 na 31.12.2022.


Alisema Shari akiwa na nia ovu alitumia madaraka vibaya. Kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa sheria ya kupambana na rushwa(PCCA) kifungu cha 31 sura ya 329 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022. Kwani kwa makusudi huku akijua kitendo hicho hakikubaliki hakupeleka fedha kwa mhasibu wa halmashauri ya Mbozi kwa kutoingiza kwenye akaunti ya halmashauri hiyo kiasi cha shilingi 5,044,599.


" Mheshimiwa hakimu, kosa hili ni kinyume na agizo namba 37(2) na 50(5) la randama ya fedha za serikali za mitaa ya mwaka 2009 ," alisema Mtaki.


Alisema mshitakiwa huyo pia anatuhumiwa kufanya ubadhirifu na kufuja fedha kiasi cha shilingi 5,044,599 za halmashauri ya wilaya ya Mbozi. Kitendo ambacho ni kosa kwa mujibu wa PCCA kifungu cha 28(1) sura ya 329 ambayo ilifanyiwa marejeo mwaka 2022. Ambapo akiwa mtumishi wa umma, huku fedha hizo zikiwa mikononi mwake alifuja na kufanya ubadhirifu huo kwa kufanyia matumizi binafsi.


Kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa hoja za awali tarehe 12.06.2024. Huku Shari ambae amekana kutenda makosa hayo akiendelea kubaki mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Post a Comment

0 Comments