TAKUKURU Songwe " yasitukia mchezo mchafu " yaokoa shilingi 16 milioni, yataja mikakati ya Aprili-Juni 2024.
Na AHMAD MMOW.
Katika kufuatilia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa wa Songwe, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) katika mkoa huo imebaini mapungufu ya upimaji kazi ambayo yamefanyika katika mradi wa ujenzi wa maegesho ya magari makubwa (malori) katika kata ya Chimbuya wilaya ya Mbozi. Mapungufu ambayo yalisababisha mkandarasi anaetekeleza mradi huo alipwe fedha za kazi ambazo hakufanya.
Hayo yameelezwa leo mjini Vwawa na naibu mkuu wa TAKUKURU wa mkoa wa Songwe, Buddy Msigala alipozungumza na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali waliopo mkoani humo.
Naibu mkuu huyo wa TAKUKURU wa mkoa wa Songwe amesema mapungufu hayo yangempa faida isiyotokana na kazi mkandarasi huyo kutokana na kulipwa fedha ambazo hakufanyia kazi. Kwani tayari alilipwa shilingi 1.24 milioni (shilingi 1,248,500) za ziada katika malipo ambayo tayari yamefanyika yenye jumla ya kiasi cha shilingi 116.78 milioni ( shilingi 116,782,500) kwenye mradi wenye thamani ya shilingi 1.867 bilioni (1,867,801,400). Mradi ambao ni baina ya Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) na mkandarasi ambae ni kampuni ya ujenzi ya MEHRAB (MHRAB CONSTRUCTION).
" Ufuatiliaji ulibaini kuwa mapungufu hayo yalisababishwa na uzembe wa msimamizi wa mradi kutoka TANROADS ambae pia alihusika na upimaji wa kazi ambazo mkandarasi alitakiwa kufanya," alisema Msigala.
Alibainisha kwamba TAKUKURU iwapo isingebaini mapungufu hayo mkandarasi huyo angelipwa shilingi 16.00 milioni (shilingi 16,000 000). Ambapo baada ya ufuatiliaji huo, TANROADS ilikiri kufanyika na kuwepo mapungufu hayo ambayo yangeisababishia hasara serikali.
Msigala alisema TANROADS licha ya kukiri kufanyika na kuwepo mapungufu hayo lakini pia imeahidi kurekebisha upimaji, muda wa malipo na mkandarasi kukatwa fedha za ziada alizolipwa.
" Kwakuwa mradi huo unaendelea, TAKUKURU itaendelea kufuatilia mradi huo ili mapungufu hayo yasijirudie," alisisitiza Msigala.
Aidha Msigala amesema taasisi hiyo pia imefuatilia utekelezaji wa miradi kumi na saba yenye thamani ya kiasi cha shilingi bilioni 17.351(17,351,122,838.21). Huku akisema kuwa miradi hiyo ipo katika sekta za elimu, maji, afya na miundo mbinu. Ambapo ufuatiliaji huo pia ulibaini miradi mitano kati ya hiyo kumi na saba yenye thamani kiasi cha shilingi 6.239 bilioni ( shilingi 6,239,736,117.21) ina mapungufu ya kiufundi. Huku pia akiweka wazi kwamba TAKUKURU imewashauri wahusika kufanyia marekebisho mapungufu hayo.
Katika hatua nyingine taasisi hiyo yenye dhamana ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoani Songwe kwa mujibu wa naibu mkuu huyo wa TAKUKURU katika kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka 2024 imepanga kutoa elimu inayohusu rushwa na kutatua kero za wananchi kupitia programu ya TAKUKURU RAFIKI, kufanya ukaguzi wa miradi katika sekta za kilimo, maji, mifugo, na ufuatiliaji wa utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa kwenye uchambuzi wa mifumo na ufuatiliaji wa rasilimali za umma.
MWISHO
0 Comments