ALAT MKOA WA LINDI YAIPONGEZA HALMASHAURI YA NACHINGWEA UJENZI WA MAABARA YA KISASA.

Na Ahmad Mmow, Nachingwea.

Halmashauri ya wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi imepongezwa kwa ujenzi wa maabara ya kisasa katikà hospitali ya wilaya hiyo na matumizi mazuri ya fedha zilizotolewa na serikali kuu kwa ajili ya uboreshaji  wa miundo mbinu ya hospitali kongwe zilizopo hapa nchini.

Pongezi hizo ziliyolewa  na mwenyekiti wa Jumuia ya Tawala za Serikali za Mitaa Tanzania(ALAT) wa mkoa wa Lindi, Andrew Chikongwe.

Chingongwe ambae  pia ni mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa alitoa pongezi hizo jana akiwa na wajumbe wa Jumuia hiyo mara baada ya kukagua ujenzi wa maabara hiyo ili kujiridhisha na matumizi ya fedha za uboreshaji wa hospitali kongwe  nchini.

 Chikongwe alisema kazi iliyofanywa na halmashauri hiyo ya kupigiwa mfano. Kwani wameona na kujifunza mengi. Hasa ubora wa maabara hiyo ya hospitali ya wilaya. Ambayo kutokana na ubora huo imepata hadhi ya nyota tatu.

" Tumeona maabara nzuri ya kisasa yenye hadhi ya nyota tatu. Sio jambo la masihara hata kidogo kuwahi kutokea, hasa katika ukanda wa Kusini kwa hospitali za halmashauri kupata hadhi ya nyota tatu," alisema Chikongwe.

Awali akitoa taarifa ya uboreshaji huo, kaimu mganga mkuu wa hospitali ya wilaya ya Nachingwea, Dkt Ramadhan Maige ambae pamoja na mambo mengine aliishukuru serikali kwa kupeleka fedha nyingi za uboreshaji wa huduma za afya wilayani humo alisema halmashauri hiyo ni miongoni mwa halmashauri zilizopokea fedha kutoka serikali kuu kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya hospitali kongwe zilizopo hapa nchini. Ambapo halmashauri hiyo ilipokea shilingi milioni mia tisa.

Alisema kiasi hicho cha fedha kimetumika kwa ujenzi wa kichomea taka, jengo la kufulia nguo, jengo la wagonjwa wa nje lenye nafasi kubwa(OPD) pamoja na maabara hiyo ya kisasa ambayo ni bora ikilinganishwa na ya awali. Kwani maabara hiyo ina uwezo wa kuchukua vipimo zaidi ya themanini. Ambapo awali ilikuwa inachukua chini ya vipimo sabini.

Dkt Ramadhan alibainisha kwamba jengo la maabara hiyo limezingatia usiri na nafasi ya kutoa vipimo kwa wakati kulingana na tatizo husika kwa kutumia vifaa vya kisasa.

" Tunampongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi za uboreshaji wa huduma za afya katika wilaya yetu ya Nachingwea," alisema Dkt Ramadhan.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi ambao ndio watumiaji wa hospitali hiyo, wakiwamo Zainab Yusufu na Stephano  Raymond walisema uboreshwaji huo umesababisha utolewaji huduma bora na  zenye uhakika katika hospitali hiyo ikilinganishwa na awali kabla ya maboresho hayo.

Walisema kabla ya maboresho hayo baadhi ya vipimo havikuwepo. Hali ambayo ilisababisha kukosekana matibabu sahihi kwa baadhi ya magonjwa. Kwani yalikuwa hayaonekani kutokana na kukosekana vifaa vya kupimia magonjwa hayo.

MWISHO

Post a Comment

0 Comments