UWT NACHINGWEA YALIA NA MALEZI YA WATOTO NA UKATILI WA KIJINSIA.


 UWT Nachingwea yalia na malezi ya watoto na ukatili wa kijnsia. 

Na Ahmad Mmow, Lindi.

Kukosekana kwa malezi sahihi kumetajwa kuwa ni miongoni mwa sababu za mmomonyoko wa maadili na ukatili wa kijinsia.

Hayo yalielezwa na mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Tanzania wa Chama Cha Mapinduzi(UWT-CCM) wa wilaya ya Nachingwea, Bi Salima Chilima,  jana tarehe 29.03.2025 katika kijiji cha Mpiruka A, halmashauri ya wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi kwenye maadhimisho ya siku ya wanawake duniani kwa ngazi ya kata ya Mpiruka.

Chilima alisema chanzo cha mmomonyoko wa maadili na ukatili wa kijinsia ni wazazi hasa wanawake kushindwa kutimiza wajibu wao wa kulea. Badala yake wanatoa matunzo kwa watoto. 

Alibainisha kwamba wazazi wengi wanajitahidi kuwapa mahitaji ya msingi watoto wao. Ikiwamo malazi, chakula, mavazi na malazi mambo ambayo ni matunzo nasio malezi. Kwani malezi ni mzazi kumfundisha mtoto tabia njema, kufanya kazi halali ili kujipatia mapato, kuepuka vitendo vya kihalifu na kufuatilia mwendendo na tabia ya mtoto.

Alisema jukumu la kulea watoto limewashinda wazazi wengi. Matokeo ya kushindwa huko ni watoto kutokuwa na tabia njema. Hali inayosababisha wajiingize kwenye vitendo vya kihalifu kupitia vitendo na kauli za watoto hao.

"Wazazi kushindwa kufuatilia mienendo ya watoto wao kunasababisha watoto hao kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia au kujiingiza kwenye vitendo viovu. Mtoto afuatiliwi anajelea mwenyewe unachojali ni kumpa chakula, nguo na sehemu ya kulala. Mengine unonq hayakuhusu, ujue unamtunza tu mwanao lakini humlei," alisisitiza Chilima.

Aidha mwenyekiti huyo wa UWT-CCM wa wilaya ya Nachingwea  aliwaasa wanawake kuacha vitendo vya ukatili wa kijinsia. Akibanisha kwamba hata wanawake wanawafanyia ukatili wa kijinsia wanaume.

" Kuondoka nyumbani bila kumuaga au kuruhusiwa na mume wako ni ukatili wa kijinsia pia," alisema Chilima.

Nae diwani wa viti maalumu(CCM) wa kata hiyo ya Mpiruka, Veronica Makota aliwaasa wanaweke waliopo katika kata hiyo wapendane na kushirikiana. Kwani miongoni mwa sababu zinazowaangusha wanawake ni kukosekana kwa umoja na upendo baina yao.

Alisema iwapo wanawake wangependana na kushirikiana wasingeshindwa kwenye chaguzi dhidi ya wanaume ambao idadi yao ni ndogo kuliko wanawake.

MWISHO.

Post a Comment

0 Comments