DIWANI MAKOTA ASEMA MUDA WA WANAWAKE KUFANYWA MADARAJA UMEKWISHA.


 Diwani Makota asema muda wa wanawake kufanywa madaraja umekwisha.

Na Ahmad Mmow,  Nachingwea. 

Wanawake waliopo katika kata ya Mpiruka halmashauri ya wilaya ya Nachingwea mkoa wa Lindi  wameaswa kupendana na kushirikiana kwa dhati badala ya kutengana na kujengeana chuki.

Wito huo ulitolewa jana katika kijiji cha Mpiruka A, na diwani wa viti maalumu(CCM) wa kata ya Mpiruka, Mheshimiwa Veronica Makota wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake dunia. Ambayo katika kata hiyo yaliadhimishwa jana tarehe 28.03.2025.

Alisema kinachowaangusha wanawake ni kutojiamini, kutopendana na kutoshirikiana. Iwapo watabadilika na kuacha tabia hizo wataweza kufanya makubwa.

Alibainisha kwamba muda wa wanawake kufanywa madaraja ya wanaume kufikia malengo yao ya kisiasa na kuingia kwenye vikao vya maamuzi umekwisha. Na kwamba fikra za kwamba adui wa mwanamke ni mwanamke waondokane nazo. Bali adui wa mwanamke kufikia malengo ni mwanaume.

" Wakati Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anashika madaraka ya U Rais watu wengi walikuwa na wasiwasi kutokana na yeye kuwa mwanamke. Kwahiyo asingeimudu nafasi ya U Rais. Lakini mambo anayofanya yamekuwa makubwa na mazuri sana kuliko hata wanaume," alisema Makota.

Kutokana na ukweli huo, diwani huyo aliwaasa pia wanawake wajitokeze kugombea nafasi za udiwani na ubunge kwa wale watakaopitia   Chama Cha Mapinduzi. Kwani fomu ya mgombea wa chama hicho ni moja tu, ambayo ni ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassani

Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii wa halmashauri ya wilaya ya Nachingwea,  Christina Makula alitoa wito kwa jamii kuacha vitendo vya ukatili wa kijinsia, hasa kwa watoto.

Alibainisha kwamba mashauri mengi yanayopelekwa katika ofisi ya ustawi wa jamii ni ukatili wa kijinsia. Hasa kuhusu ulawiti na ubakaji kwa watoto.

Post a Comment

0 Comments