NAPOA yawaasa wazazi kuwalea na kuwafundisha watoto maadili mema.
Na Ahmad Mmow, Nachingwea.
KUTOKANA na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani Nachingwea mkoa wa Lindi, shirika lisilo la kiserikali la Nachingwea Paralegal Aid Organization (NAPAO) limeamua kutoa elimu ya sheria ya mtoto. Ambapo leo tarehe 17.06.2024 limetoa elimu hiyo kwa wananchi wa kijiji cha Mkonjela Chini ili jamii itambue haki za watoto na wajibu wao katika malezi.
Akizungumza na wananchi hao kuelekea siku ya mtoto wa Afrika. Mkurugenzi wa Shirika hilo ambalo sio la kiserekali ambaye pia ni msaidizi wa kisheria,Sabrina Dossa alisema wazazi lazima watambue haki za watoto kama vile kuwapa ulinzi,elimu na mahitaji yote muhimu.
Alisema wazazi wanapaswa kufichua matendo yote ya ukatili wa kijinsia,kama vile ulawiti, ubakaji na ndoa za utotoni ili kuwa na kizazi bora kwa faida ya familia na taifa kwa ujumla.
Alitoa wito kwa wazazi ,walezi na jamii kuwa makini katika malezi kwa kuwafunza watoto mila na tamaduni zao na kuwapatia mafundisho yenye maadili mema kwa jamii na maisha yao kwa ujumla.
Kwa upande wake ofisa habari na mawasiliano wa shirika hilo, Christopher Lilai alisema kuwa shirika linatoa msaada wa kisheria,ushauri wa kisheria kwa jamii, na usuluhishaji wa migogoro kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kifedha wa kugharamia.
"Shirika letu linatoa huduma za kisheria bila malipo yeyote kwa wale ambao hawana uwezo lengo ni kumfanya mwananchi apate haki yake bila kuathiriwa na umaskini"alisema Lilai.
Nae alitoa wito kwa kila mwananchi anae hitaji msaada huo aende katika ofisi za shirika hilo au kwa wasaidizi wa kisheria waliopo kwenye kata 14 zilizopo ndani ya wilaya ya Nachingwea.
Mmoja wa wazazi wa kijijini hapo, Zuhura Ungele alisema kwamba, baaadhi ya wazazi wanawagopa watoto wao wanaosoma sekondari hivyo kusababisha watoto wengi kuwadharau wazazi wao baada ya kufika kidato cha nne na kuendelea. Kwani wanajiona ni wasomi kuliko wazazi wao.
Mwananchi huyo alisema mwenendo wa maisha ya watoto sio mzuri. Kwani asilimia kubwa yanakiuka maadili ya watanzania. Hivyo alitoa wito kwa watoto wote kuanza kuwajibika kwa wazazi wao ili wapate malezi bora na mema.
0 Comments