MLINZI WA UWANJA WA NDEGE AITWA NGUVUNI KWA WIZI WA PIKIPIKI.

 



Mlinzi wa uwanja wa ndege atiwa nguvuni kwa wizi wa pikipiki

Na Ahmad Mmow, Lindi.

Jeshi la Polisi mkoani Lindi, kwa kushirikiana na wenzao wa Mkoa wa Mtwara, Septemba 20,2025 limemkamata mlinzi wa uwanja wa ndege wa Kilwa Masoko, Shaha Athuman Mohamed (20) kwa tuhuma ya wizi wa pikipiki aina ya TVS yenye namba za usajili STN 2790, mali ya uwanja huo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Lindi, Kamishna Msaidizi wa Polisi(ACP) John Imori, mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo mnamo Septemba 16, 2025, akiwa zamu kazini katika uwanja huo. 

Kamanda Imori amesema kwamba baada ya kutekeleza uhalifu huo alitoweka na pikipiki hiyo na kuacha kazi bila taarifa.

 Amesema, baada ya tukio hilo mamlaka ya uwanja huo ilifungua jalada la kesi lenye namba KLM/IR/429/2025 katika Kituo cha Polisi Kilwa Masoko kwa kosa la wizi. Ndipo jeshi hilo la polisi lilianza msako mkali na kufanikiwa kumnasa mtuhumiwa huyo.

Shaha alikamatwa katika mtaa wa Mkomaindo, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, akiwa katika harakati za kuuza pikipiki hiyo.

Kamanda Imori amebainisha kwamba Kukamatwa kwa mlinzi huyo kulifanikishwa na mtego uliowekwa na askari polisi, ambao ulisababisha kumtia mbaroni.

"Baada ya kukamatwa, Shaha aliwaongoza askari hadi eneo alilokuwa ameificha pikipiki hiyo, ambapo alionyesha namba kamili za usajili kabla ya pikipiki hiyo kupatikana kichakani," alisema Kamanda Imori.

Mtuhumiwa huyo ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya ulinzi ya INSIGHT aliyekuwa akilinda katika uwanja wa ndege wa Kilwa Masoko, anatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada upelelezi kukamilika.

Kamanda huyo wa polisi wa mkoa(RPC) ametoa wito kwa wananchi waendelee kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za uhalifu ili kuimarisha usalama katika maeneo yao.

Post a Comment

0 Comments