TAKUKURU SONGWE YALIA NA UONGOZI NA USIMAMIZI MBAYA KATIKA VYAMA VYA USHIRIKA


 TAKUKURU Songwe yalia na uongozi na usimamizi mbaya katika vyama vya ushirika.

Na Ahmad Mmow. 

Uongozi mbaya na usimamizi hafifu wa viongozi na utendaji mbaya wa watumishi wa baadhi ya vyama vya ushirika ni changamoto inayosababisha kukosekana mafanikio katika baadhi ya vyama vya ushirika.

Hayo yameelezwa leo mjini vwawa,wilaya ya Mbozi, na naibu mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU ) mkoa wa Songwe, Buddy Msigala wakati wa semina kwa wajumbe wa mkutano mkuu wa chama vikuu cha ushirika mkoa wa Songwe(SORECU).

Amesema uongozi mbaya na usimamizi hafifu ni changamoto kubwa inayovikumba vyama vingi vya ushirika. Kwani katika baadhi ya vyama viongozi hawana ufanisi katika kusimamia rasilimali na shughuli za ushirika. Hali inayosababisha matumizi mabaya ya fedha, wizi na upotevu wa mali.

Amebainisha kwamba usimamizi mbaya pia unasababisha upotevu wa imani miongoni mwa wanachama. Hivyo kuathiri utendaji wa vyama.

Amesema vyama vya ushirika vikiwa na mfumo mzuri wa utawala na uongozi unaojali masilahi masilahi ya wanachama wake kwakuwa na usimamizi mzuri wanachama watapata huduma bora na watanufaika na ushirika.

" Kwajumla ushirika ambao viongozi na watendaji wakisimamia vizuri utatoa fursa nyingi za maendeleo kwa wanachama na wananchi kwa jumla. Hasa kwa wale walio vijijini na wenye vipato vya chini," Msigala alisisitiza.

Naibu mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa wa Songwe ameweka wazi kwakusema baadhi ya vyama vya ushirika kuna viongozi na watendaji wanatuhumiwa kutumia vibaya fedha za wanachama(fedha za ushirika) kwa masilahi binafsi. Kitendo kinachosababisha wanachama kupoteza imani kwa vyama vya ushirika. Hivyo kupunguza ushiriki wao.

Aidha Msigala aliwaasa wanachama hao waepuke migogoro isiyo ya lazima. Kwani migogoro ndani ya vyama vya ushirika ni changamoto nyingine inayoathiri malengo ya ushirika.

" Migogoro inaweza kusababishwa na tofauti za kimaslahi usimamizi mbaya au malalamiko kuhusu usawa katika mgawanyo wa faida. Kwahiyo nawasihi sana epukeni yanayoweza kusababisha migogoro.

Mbali na hayo naibu mkuu huyo wa TAKUKURU, aliwaasa wanachama hao waepuke kutanguliza ubinafsi, kutokuwa waaminifu na waadilifu na wazingatie maslahi ya wanachama. Huku akiwaonya wasitumike kama madaraja kwa watoa rushwa ambao wanafuta uongozi kwa njia ya hongo ili wachaguliwe kuwa viongozi wa chama hicho.

Semina hiyo ni maandalizi ya mkutano mkuu wa chama hicho cha ushirika cha Songwe(SORECU) ambao pamoja na mambo mengine utatumika kuwachagua viongozi 

 ambao wataunda bodi ya chama kikuu hicho.

Post a Comment

0 Comments