Nambole: CCM kinafikiria amani na maendeleo.
Na Ahmad Mmow, Nachingwea.
Chama Cha Mapinduzi(CCM)Wilayani Nachingwea kimesema kinafikiria zaidi suala la amani na maendeleo kwa wananchi badala ya vurugu.
Leo akizungumza na baadhi ya wakulima wa kata ya Mpiruka ambao wanadhamiria kuanzisha chama cha msingi cha ushirika(AMCOS). Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Nachingwea, Longnus Nambole amesema fikra za chama hicho kwa wananchi ni kuona wanaishi kwa amani, utulivu na wanapata maendeleo.
Nambole ambaye aliyasema hayo kufuatia kilio cha wakulima cha kulima hao ambao walimueleza azima yao ya kuanzisha AMCOS, alisema Chama Cha Mapinduzi kina amini katika mazungumzo na majadiliano katika kuzitafutia utatuzi changamoto. Kwani dhamira ya chama hicho ni kuona wananchi wanaishi kwa amani na wanapata maendeleo.
Amesema wananchi wanakila sababu ya kuepuka migogoro inayoweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani. Badala yake watumie njia za kistaharabu iwapo wataona madai yao hayafanyiwi kazi.
"Chama Cha Mapinduzi kinafikiria amani na maendeleo. Hakipendi kuona vurugu na umwagaji damu. Kukiwa na changamoto mnazungumza na kujadiliana na kupata ufumbuzi bila kutumia nguvu na vurugu,"alisisitiza Nambole.
Kiongozi huyo wa CCM wilayani Nachingwea licha ya kuahidi atafikisha ombi la wakulima hao kwa mamlaka husika amesema ni wakati wa kuunga mkono fikra za wananchi ambao wana nia njema ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kujiletea maendeleo.
" Tuzungumzie ujenzi wa viwanja vya ndege, ujenzi wa barabara, viwanja vya michezo na mambo mengine ya maendeleo. Sio kuzungumzia vurugu na uvunjifu wa amani. Nimewasikia, nimeelewa na nitafanyia kazi. Bali nanyi zingatie, simamieni na mdumishe, amani na umoja," Nambole aliwaahidi na kuwa rai wakulima hao.
Kwa upande wao wakulima hao walisema, walimuomba mwenyekiti huyo wazungumze nae ili kumueleza azima yao ya kuanzisha AMCOS kwa madai kwamba inakwamishwa.
Salum Mkitage ambae ni mmoja wa wakulima hao alisema azima yao ya kuanzisha chama inadalili ya kukwamishwa. Kwani juhudi za kuanzisha zina miaka sita. Hata hivyo kuna mazingira ya kukwamishwa. Huku akidai hawajui sababu.
Maelezo ambayo yaliungwa mkono na mkulima Mwanahawa Kinunda ambae alisema licha ya juhudi kubwa walizofanya lakini kuna dalili za kile alichoita zengwe kutoka kwa mamlaka. Hali ambayo imesababisha wamuombe mwenyekiti huyo aingilie kati. Kwani Chama Mapinduzi ndicho kimeunda serikali na ilani yake ya uchaguzi ndiyo inayotekelezwa.
Nae mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mpiruka A, Awadh Ngomo alisema kuna haja ya wakulima hao kusaidiwa ili waanzishe chama. Kwani wamehangaika kwa muda mrefu. Na hajui ni kwanini azima yao inakwamishwa.
Kata ya Mpiruka ina chama kimoja cha msingi cha ushirika(AMCOS) kinachoitwa Ukombozi(Ukombozi AMCOS) ambacho ni miongoni mwa vyama vilivyo chini ya chama kikuu cha ushirika cha RUNALI.

0 Comments